Saturday, December 28, 2013

Aliyekuwa mchezaji wa zamani na Kocha wa makipa Simba, marehemu James Kisaka azikwa kwao Muheza Tanga


Jaji wa Mahakama ya Jumuia ya Afrika Mashariki (wa pili kulia na suti nyeusi), John Mkwawa akiuaga mwili wa marehemu James Kisaka leo, nyumbani kwao Muhenza, mkoani Tanga wakati wa shughuli za mazishi yake.
 Ndugu wakimlilia mpedwa wao, James Kisaka wakati wa mazishi yake Muheza, Tanga leo.
Padre wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Tanga, Mtaa wa Lusanga kwa Yesu, akitoa maneo ya kuagwa kwa mwili wa marehemu James Kisaka, wakati wa mazishi yake leo.
 Padri wa Kanisa la Anglican, Aidano Kamote akiuaga mwili wa James Kisaka.
Waombolezaji wakishirikiana kuuingiza kaburini mwili wa marehemu James Kisaka, wakati wa mazishi yake, Muheza Tanga.
Wapenzi wa mchezo wa pira wa miguuu, Juma Mgunda wa Coastal Union (kulia) na mwenzake ambaye jina lake halikuweza kupatikana, wakiwa wanaonekana na huzuni kufuatia kifo cha aliyekuwa mchezaji mwenzao, wakati wa miaka ya 1980, James Kisaka aliyedakia Simba na kisha kuwa kocha wa makipa wa timu hiyo hivi karibuni. (Picha zote na Dotto Mwaibale)

Thursday, December 26, 2013

Ibada ya Krismasi kwa Makanisa ya Azania Front na St. Joseph ilivyoendeshwa jijini Dar es Salaam


Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, akiwa nje ya Kanisa, akiwaombea waumini wa kanisa hilo, usharika wa Azania Front, Dar es Salaam, mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Krismasi, kanisani hapo leo.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, akiwatakia heri ya Krismasi waumini wa kanisa hilo, usharika wa Azania Front, Dar es Salaam, mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Krismasi, kanisani hapo leo. Kulia ni Mchungaji Charles Mzinga.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, akiwapa mkono wa Krismasi waumini wa kanisa hilo, usharika wa Azania Front, Dar es Salaam, mara baada ya ibada iliyofanyika kanisani hapo leo.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, akizungumza na waumini wa kanisa hilo, usharika wa Azania Front, Dar es Salaam, mara baada ya ibada Krismasi, iliyofanyika kanisani hapo leo.
Mchungaji akiwa katika mahubiri kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam leo.
Waumini wa Kanisa Katoliki, wakiwa katika ibada ya Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam leo

Tuesday, December 24, 2013

ANGALI PICHA KIBAO ZA JOSE CHAMILEON NA JAMBO SQUARD NA LEO NDI WATAWASHA MOTO USIKU HUU CCM KIRUMBA

Mwanamuziki mahiri toka nchini Uganda Dr. Jose Chameleone akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusiana na Tamasha lililopewa jina la 'Badilisha Concert' litakalofayika leo 24 dec 2013 katika uwanja wa CCM Kirumba kuanzia saa 12 jioni hadi majogoo kama sehemu ya kuikaribisha sikukuu ya Christmass. Pembeni yake anaonekana meneja wake na mwisho kabisa kulia ni mmoja wa wadhamini wa Tamasha hilo Mr. James Njuu wa K Vant Gin.
Mwanamuziki mahiri toka nchini Uganda Dr. Jose Chameleone akisalimiana na mmoja kati ya wasanii wa Jambo Squard mbele kidogo ni Dogo Dee na mwisho kabisa (kushoto) katika mstari ni mwanamuziki Bob Haisa ambao wamefika kumpa sapoti katika show ya Badilisha Concert itakayofanyika leo CCM Kirumba Mwanza. 
Mwanamuziki mahiri toka nchini Uganda Dr. Jose Chameleone akisalimiana na ndugu zake wasanii wa Tanzania waliofika leo kuzungumza na waandishi wa habari katika Hotel Gold Crest Mwanza.
Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Denis (kushoto) kutoka Silver Intertainment amesema kuwa kampuni yake imeamua kuweka kiwango kidogo cha kiingilio ili watu wote wa Kanda ya Ziwa waipate zawadi ya mwaka kushuhudia burudani kali.
"Zawadi nyingi huwekwa kwenye boxi lakini hii yaani mimi ni zawadi iliyo nje ya boxi maalum kwa wakazi wa Mwanza" pia Jose Chameleone anasema kuwa najivunia kuwa Mwanza mji ambao kwangu ni sawa na nyumbani.
Jose Chameleone amekwepa kulizungumzia suala lake la hivi majuzi kukumbatiana na mdogo wake Weasal na binamu yake Radio ile hali walikuwa kwenye bifu kali akisema yote yatafanyika lakini undugu utabaki pale pale akisita kuendelea kulizungumzia suala hilo kwa undani akisema hawezi kuzungumzia masuala ya familia nje ya familia anaheshimu utamaduni wa kiafrika.



Jose Chameleone akiwa na wasanii wa Tanzania kutoka kushoto ni Bob Haisa, King Houston, Chemeleone (mwenyewe) Dogo Dee, Chuse, na Jambo Squard team.
Jose Chameleone akiwa na wadhamini waliosimamia mzigo ukasimama.
Take two na wadhamini.
Jose akiwa na wanahabari wa Mwanza.
Uskose usiku wa leo ndani ya uwanja wa CCM Kirumba.

TAARIFA KAMILI KUHUSU BEI MPYA ZA UMEME ZITAKAZOANZA KUTUMIKA TAREHE 1/1/2014



Tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liliwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya,
kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania. Aidha, TANESCO iliomba kuidhinishwa viwango vya gharama za kuunganisha umeme vinavyozingatia ruzuku inaliyotolewa na Serikali, na kuidhinishwa tozo mbalimbali kwa huduma zitolewazo na TANESCO.

Kwa mujibu wa TANESCO, kupitishwa kwa maombi haya kutaliwezesha Shirika (a) kupata fedha za uendeshaji na uwekezaji wa miundombinu, (b) kulifanya Shirika liweze kukopesheka na hivyo kuwezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu, (c) kuliwezesha Shirika kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya Taifa, na (d) kuongeza uwezo wa kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu iliyopo ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma za umeme wa uhakika kwa wateja.

Itakumbukwa kwamba bei za umeme zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa mwezi Januari 2012. Bei hizo zilipanda kwa asilimia 40.29 ikilinganishwa na maombi ya TANESCO ambapo ilipendekeza bei zipande kwa wastani wa asilimia 155. Sababu ilikuwa ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kulikosababishwa na hali ya ukame katika maeneo yanayotiririsha maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme, toka mwaka 2011. Hali hiyo ilipelekea TANESCO kulazimika kununua umeme kwa gharama kutoka kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power Producers). Hali ya maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme bado sio nzuri na hivyo TANESCO itaendelea kununua umeme kutoka kwa wazalishaji wa dharura (Emergency Power Producers).

USHIRIKISHWAJI WA WADAUKulingana na Kifungu Na. 19(2) (h) cha Sheria ya EWURA, Mamlaka ilifanya Taftishi ili kupata maoni juu ya ombi la kurekebisha bei za umeme. Ukusanyaji wa maoni ulihusisha pia mikutano minne (4) iliyofanyika Iringa na Shinyanga tarehe 15 Novemba 2013, Bagamoyo tarehe 20 Novemba na kuhitimishwa Dar es Salaam tarehe 22 Novemba 2013. Aidha, tarehe 6 Desemba 2013, EWURA iliitisha mkutano wa mwisho wa wadau wakiwemo wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini(MEM), TANESCO, Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, Baraza la Watumiaji na Baraza la Ushauri la Serikali, Umoja wa Wazalishaji wa Saruji wa Afrika Mashariki, na kiwanda cha ALAF. Katika mkutano huo EWURA iliwasilisha mwelekeo wa maamuzi kuhusu maombi ya TANESCO na namna zilivyokokotolewa. Wadau walipewa fursa ya kutoa maoni yao kuhusu mwelekeo wa bei na maoni yao yamezingatiwa katika kufikia maamuzi ya mwisho.

UCHAMBUZI NA UAMUZIKwa kufuata sheria na kanuni zinazoelekeza kuhusu uchambuzi wa bei ya umeme, EWURA ilifanya uchambuzi wa kifedha na kiufundi ili kubaini uwezo wa TANESCO katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Uchambuzi uliangalia utendaji wa Shirika la TANESCO katika miaka iliyopita na pia iliangalia majukumu yanayoikabili TANESCO katika miaka mitatu ijayo. EWURA imebaini kwamba hali ya kifedha ya Shirika la Umeme sio nzuri. Shirika limeendelea kupata hasara, ambayo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 47.3 katika mwaka 2010 na kufikia shilingi bilioni 223.4 mwishoni mwa mwaka 2012. Pamoja na mapungufu ya kiufanisi, sababu kubwa ya ongezeko la hasara ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa umeme ambao TANESCO inanunua kutoka kwa wazalishaji binafsi. Hali hii imelifanya shirika kushindwa kulipa madeni yake ya muda mfupi na ya muda mrefu, ambayo yamelibikizwa na kufikia TZS 456.8 bilioni tarehe 22 Novemba 2013, hali ambayo inatishia uendelevu wa huduma ya umeme hapa nchini.

Mamlaka imetumia Kanuni ya Ukokotoaji wa Bei kama ilivyopendekezwa na AF-MERCADOS wakati wa kukokotoa mahitaji ya mapato ya TANESCO. Kanuni hiyo inawezesha kukokotoa bei zinazolandana na gharama halisi kwenye mfumo wa umeme na kuzigawa kwenye makundi ya watumiaji umeme, kadiri kila kundi linavyosababisha gharama kwenye mfumo wa umeme kwa mujibu wa mahitaji ya Sheria ya Umeme ya 2008 Kifungu cha 23(2)(f).

EWURA imejiridhisha kwamba, ufumbuzi wa matatizo ya kifedha ya TANESCO, unahitaji njia/mikakati miwili itekelezwe kwa pamoja:
kuongeza bei ya umeme ili kufikia bei inayokidhi gharama halisi (Cost Reflective Tariff); na
TANESCO kupata mkopo wa gharama nafuu ama ruzuku kutoka Serikalini ili kulipa limbikizo la madeni ya Shirika.

Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja, kama ifuatavyo:

Kundi D1: Hili ni kundi la wateja wadogo wa majumbani, hasa vijijini, ambao hutumia wastani usiozidi wa Uniti 75 kwa mwezi. EWURA imeongeza wigo wa mahitaji ya umeme na kufikia uniti 75 kwa mwezi, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wateja wa TANESCO wanaoweza kulipa kidogo kwa matumizi ya umeme kwa kiwango hicho, na pia kuwahamasisha kutumie zaidi umeme. Awali kundi hili lilikuwa linatunia wastani wa matumizi ya uniti 50 kwa mwezi. Bei mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja, kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na ongezeko la shilingi 40.

Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji wakubwa wa umeme majumbani, biashara ndogondogo, mashine za kukoboa na kusaga nafaka, taa za barabarani, mabango n.k. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa uniti moja, ikiwa ni ongezeko la Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO ilipendekeza ongezeko la shilingi 131.

Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji umeme wa kawaida ambao hupimwa katika msongo wa volti 400, na ambao matumizi yao ya wastani kwa mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja wafanyabiashara kubwa, viwanda vya kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 73 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la shilingi 145 ya bei ya sasa.

Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja wakubwa kama viwanda vikubwa waliounganishwa katika msongo wa kati (Medium Voltage). EWURA imeidhinisha bei ya nishati kwa kiwango cha shilingi 166 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 45 ya bei ya sasa. TANESCO walipendekeza ongezeko la shilingi 148 kwa uniti moja.

Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu (High Voltage – Voti 66,000 na zaidi) ikiwa ni pamoja na ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement. Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 159 kwa uniti moja, sawa na ongezeko la shilingi 53 la bei ya sasa. TANESCO waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa uniti moja.

Bei ya umeme itakuwa inarekebishwa kila baada ya miezi mitatu kulingana na mabadiliko ya kiwango na bei za mafuta; mfumuko wa bei, mabadiliko ya thamani ya fedha, na upatikanaji wa ruzuku toka Serikalini.

Vilevile, TANESCO inatakiwa kutekeleza miradi ya uwekezaji iliyoainishwa kwa kutumia fedha zitakazokusanywa kutokana na bei zilizoidhinishwa. EWURA inaweza kurekebisha bei ya umeme ya TANESCO kila mwisho wa mwaka 2014 na/au mwaka 2015 endapo TANESCO itashindwa kutekeleza miradi iliyotajwa katika Jedwali husika. Marekebisho hayo yatatokana na makadirio ya gharama za miradi ambayo haikutekelezwa.

Kutokana na matazamio ya kuwa na mabadiliko makubwa katika uzalishaji wa umeme (generation mix) katika mwaka 2015 na kuendelea, kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa kwa upatikanaji wa gesi asilia, EWURA itafanya utafiti kubaini gharama halisi (Cost of Service Study) ya huduma ya umeme kwa wakati huo. Hivyo, bei zilizoidhinishwa zitatumika mpaka mwaka 2016, kama utafiti unaotazamiwa kufanywa hautakamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2015.

EWURA ililinganisha bei za umeme kwa kila Uniti, katika nchi za Afrika ya Mashariki, na kuona kuwa bado bei za umeme za Tanzania zipo chini ukilinganisha na bei za katika nchi jirani kama inavyoonyeshwa hapa chini, kwa makundi mbalimbali ya watumiaji umeme.

Pamoja na maamuzi hayo, Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA, pia iliagiza TANESCO kutekeleza yafuatayo:


  • kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo yenye gharama nafuu ("least cost merit order") na kuwasilisha ripoti kwa Mamlaka katika kila mwezi ikionyesha uzalishaji halisi na mpango wa uzalishaji kama ilivyoidhinishwa na EWURA;

  • kuhakikisha kuwa zabuni za miradi ya uzalishaji umeme zinatolewa kulingana na mahitaji kama ilivyoidhinishwa kwenye Mpango wa Umeme wa Taifa (Power System Master Plan). Miradi yote mipya lazima ipatikane kwa njia ya ushindani kwa kufuata Sheria ya Umeme, "Public Private Partnership Act", Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni husika;

  • kuwasilisha ripoti kila baada ya miezi mitatu kuhusu viashiria vya takwimu za ubora na uhakika wa umeme (supply and reliability) katika misongo ya 11kV, 33 kV, 66 kV, 132 kV, na 220 kV kwa kila mkoa kwa ajili ya uhakiki. Takwimu husika zinatakiwa kuonyesha jumla ya masaa mteja aliyokosa umeme kwa kila njia ya umeme ("feeder"), kukosekana kwa umeme kulikopangwa (planned outages), na ambao haukupangwa (unplanned outages), idadi ya matukio ya kukosa umeme katika kila "feeder", idadi ya wateja wanaohudumiwa na kila "feeder", idadi ya wateja walioathirika na katizo la umeme katika kila "feeder" na kiasi cha umeme kilichokosekana kutokana na katizo hilo (total unserved energy in kWh);

  • kuwasilisha kwa Mamlaka, katika kipindi cha miezi mitatu baada kuanza kwa Agizo hilo la Mamlaka, mpango wa utekelezaji wa "Demand Side Management Programme" ili uidhinishwe;

  • kupunguza kiwango cha upotevu wa umeme (technical and non-technical losses) katika mtandao wa usambazaji kutoka asilimia 19 ya mwaka 2012 hadi asilimia 15.1 ifikapo mwisho wa mwaka 2015;

  • kubuni mikakati ya kupambana wizi wa umeme utokanao na uunganishaji umeme usio halali, na kuondoa ucheleweshaji usio wa lazima katika kutunganisha wateja wapya;

  • kuhamisha wateja walio katika kundi la D1 kwenda T1 endapo matumizi yao ya mwezi yatazidi uniti 75 kwa miezi mitatu mfululizo;

  • kuwasilisha kwa Mamlaka, kabla au tarehe 31 Machi, 2014, Mpango wa kuwawekea wateja wake mita za LUKU na AMR ili kupunguza wateja wanaotumia mita za zamani (conventional meters);

  • kuwasilisha kwa Mamlaka, kila baada ya miezi mitatu, taarifa/ripoti ya ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wateja wake ili kuongeza mapato ya Shirika;

  • kutoa elimu kwa wateja wake kuhusu haki na wajibu wa wateja kwa mujibu wa Mkataba wa Huduma kwa Wateja na kushughulikia kero za wateja kama inavyoelekezwa katika Mkataba husika na Kanuni za Umeme;

  • kuwasilisha kwa Mamlaka, maombi ya marekebisho ya bei yatokanayo na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na ubadilikaji wa thamani ya fedha; Ukokotoaji wa marekebisho hayo utakuwa kama ulivyoainishwa katika Kanuni za Kupanga Bei za Umeme za mwaka 2013 (Electricity (Tariff Setting) Rules, 2013);

  • kuendelea kutoa taarifa kwa Mamlaka kuhusu hali ya kifedha na kiundeshaji. Taarifa hizi zitatumiwa na Mamlaka katika kutathmini utendaji wa TANESCO ikilinganishwa na mashirika mengine ya umeme katika nchi jirani ili kuboresha utendaji wake. Tathmini hii pia itatumiwa na Mamlaka katika kubaini uhalali wa maombi ya baadae ya kurekebisha bei;

  • kuwasilisha kwa Mamlaka, kabla au tarehe 31 Machi 2014, mpango wa utekelezaji wa kila sharti katika Agizo la EWURA.

Bei mpya za umeme zitaanza kutumika tarehe 1 Januari 2014. Ni matarajio ya EWURA kwamba TANESCO watatumia fursa hii kutoa huduma bora zaidi za umeme na kuhakikisha kuwa wanashughulikia malalamiko ya wateja kila yanapojitokeza ili kurejesha imani kwa Shirika la Umeme la TANESCO.

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Sunday, December 22, 2013

ZITTO KABWE AFUNIKA KIGOMA..........HII NI HOTUBA YAKE ALIYOITOA LEO KWA WANAKIGOMA



HOTUBA YA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA – 21 DESEMBA 2013
Leo nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji.

Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.

Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini, Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. Kabla ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994.

Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.

Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma.

Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma. Nimekuwa nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu. Viatu hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili kwenda la tatu. Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania.

Uwajibikaji kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote. Jamii hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya juu sana.

Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia. Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza umasikini. Demokrasia inahusu maendeleo.

Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga.

Asije mtu akasema yeye ndio kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu wa Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa makuu.

Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na sio Kigoma tu.

Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani.

Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. Hii ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia yetu.

Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.

Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.

Kutoaminiana
Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli.

Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa zetu. Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa badala ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo.

Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara nne. Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria.

Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika. Sitaingia mtego huu! Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi ninaingia katika hali ninayoilalamikia yaKUTOAMINIANA.

Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo. Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa woga.Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta. Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.

Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli
Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule.

Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake ambayo sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.

Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo! Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi.Ninasukuwa kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu; kila ninapoona akina mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu.

Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni 2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania.

Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).

Nimewatajia hapa namba chungu nzima na matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka Kigoma mpaka Dar-es-salaam!

Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana wetu. Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya viatu. Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti!

Lakini naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila sababu. Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra zake zinakuwa huru.

Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo. Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta matumaini. Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki kipya. Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha; ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo. Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania.

Mungu ibariki Tanzania.

 
 

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 14 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 21 DESEMBA, 2013



I:          UTANGULIZI 
a)          Masuala ya Jumla

Mheshimiwa Spika,
1.            Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa Dodoma kwa takriban siku 15 za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi za Mkutano wa 14 wa Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa hivi leo.

Mheshimiwa Spika,
2.            Nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Asha Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu.  Wengi wetu tunafahamu uwezo mkubwa wa Dkt. Asha Rose Migiro na bila shaka ndiyo sababu Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia sifa nzuri alizonazo. Pamoja na kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika,
3.            Tangu Mkutano wa 13 wa Bunge baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki.  Napenda kutumia fursa hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Lakini katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Azimio la Bunge kuhusu kuungana na Nchi ya Afrika Kusini, katika kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga ubaguzi wa rangi, Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba 2013.  Wote tunakubaliana kwamba huu ni msiba Mkubwa kwa Dunia nzima na hasa kwa wale wanaomfahamu Mzee Mandela na historia yake. 

4.            Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwakilisha vyema Watanzania wote katika msiba huu mkubwa wa Afrika na Dunia nzima.  Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela tarehe 15 Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa kuitangaza Tanzania Dunia nzima katika ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani Afrika katika Karne ya 20.  Ninaamini kwamba hiyo ni Historia ambayo haitafutika vizazi vingi vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga na kufuata nyayo zake.

b)            Maswali
Mheshimiwa Spika,
5.            Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kuuliza maswali ya msingi 170 na ya nyongeza 458 ambayo yote yalijibiwa na Serikali.  Aidha, maswali17 ya msingi na 15 ya nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa Mawaziri kutoa majibu ya maswali hayo kwa umahiri mkubwa.


Mheshimiwa Spika,
6.             Pamoja na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako lilikamilisha kazi kubwa zifuatazo:

Kwanza: Bunge lilijadili na kukamilisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];

Pili:                 Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge za Sekta Mtambuka.

Tatu:              Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma; na

Nne:               Kujadili Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za Kisekta.

7.            Aidha, Bunge lako Tukufu lilijadili kwa utaratibu wa Hati ya Dharura Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka 2013 [The Excise (Management and Tariff) (AmendmentBill, 2013]. Mwisho Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 ulisomwa kwa mara ya kwanza.

8.            Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili Taarifa hizo na kutoa maoni na ushauri kwa uwazi mkubwa na kwa kina. Mapendekezo na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umepokelewa na Serikali na utazingatiwa kwa uzito unaostahili.

II:         KILIMO
a)    Hali ya chakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
9.            Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa 13hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2013 katika maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula na lishe inaonesha kuwa jumla ya Watu 828,063 wanakabiliwa na upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya Tani 16,119 za chakula cha mgao kwa Halmashauri zenye mahitaji ya chakula cha msaada. Hadi kufikia tarehe 16 Disemba 2013, jumla ya Tani 13,716 zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika.Tani 2,402 zilikuwa hazijachukuliwa na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na Manyoni.

10.         Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua chakula hicho kufanya hivyo kabla ya tarehe 15 Januari 2014. Ambao hawatatekeleza maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria. Nitumie nafasi hii kuwahakikishia Wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.

b)   Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
11.         Kutokana na miezi hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua. Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika soko hapa Nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 536.86 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikiaShilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba, 2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10 kwa kilo mwezi Novemba, 2013.

12.          Pamoja na kuwepo kwa hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa na zile za kipindi kama hiki mwaka jana. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu. Halmashauri zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela wa chakula kutoka mashambani na majumbani mwa Wakulima kwa lengo la kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha.

c)    Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa

Mheshimiwa Spika,
13.         Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ilipanga kununua Tani 250,000 za nafaka. Wakala umeendelea na kazi hiyo na hadi kufikia tarehe 11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa umekwishanunua kiasi cha Tani 218,499 za nafaka sawa na Asilimia 87.4 ya kiasi kilichopangwa kununuliwa. Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Desemba, 2013, Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba ya jumla ya Tani 233,808 za nafaka.  Kati ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi na Tani 493 ni za Mtama.

14.         Wakati huo huo, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unaendelea kuhamisha chakula kutoka katika maghala yake yaliyoko katika Mikoa iliyozalisha ziada kwenda kwenye maghala yaliyoko kwenye Mikoa yenye upungufu wa chakula ili kukabiliana na mahitaji ya chakula cha msaada kitakachohitajika kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe 9 Desemba, 2013, jumla ya Tani 44,129 za Mahindi zimekwishahamishwa. Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kununua chakula katika Mikoa yenye ziada ya chakula na kukipeleka katika Mikoa yenye upungufu wa chakula.

d)   Hali Halisi ya Usambazaji wa Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
15.         Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali ilichapisha jumla ya vocha 2,796,300, kwa ajili ya pembejeo za Kilimo kwa msimu wa Kilimo wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12 Desemba, 2013, Tani 74,925 sawa na Asilimia 96 za mbolea ya kupandia na Tani 42,295 sawa na Asilimia 91 ya mbolea ya kukuzia zilikuwa zimekwishafikishwa katika Mikoa husika kulingana  na  aina  ya  mazao  yanayohitaji  mbolea  hizo. Aidha, Maghala ya Wakala wa Mbolea Jijini Dar es Salaam yana akiba ya kutosha ya mbolea hiyo. Nirejee kutoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha kuwa vocha zote zinatolewa kwa walengwa kwa wakati sambamba na aina ya pembejeo inayomlenga Mkulima husika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.







e)    Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.

Mheshimiwa Spika,
16.         Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni 109.6kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kununua Tani 250,000 za nafaka. Hadi  kufikia  tarehe  19  Desemba, 2013 NFRA ilikuwa imenunua  jumla  ya Tani 218,499  zenye  thamani  ya Shilingi Bilioni 109.25 na  kwa ajili hiyo. Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri ya wastani wa Shilingi 500/=kwa kilo ya mahindi, zoezi hilo lilikuwa na matokeo mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita na liliwavuta Wananchi wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia nafaka. Hadi sasa Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa ajili ya zoezi hilo na imehakikisha kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa NFRA wamelipwa fedha zao. Aidha, natambua kuwa NFRA ilitumia baadhi ya Wakala kukusanya nafaka hiyo kutoka kwa Wakulima na kama nilivyosema katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali inatambua kuwa Wakala hao kutoka Mikoa ya Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga wanaidai Serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8.65 Niwaombe Wakala wote wanaoidai Serikali kuendelea kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa deni hilo kwa vile kiasi cha deni lao lipo ndani ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ununuzi wa nafaka katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.

III:       MPANGO WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA

Mheshimiwa Spika,
17.         Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial Inclusion Framework). Uzinduzi wa Mpango huu ulifanywa na Malkia wa Uholanzi Mheshimiwa Máxima Zorreguieta Cerruti ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Spika,
18.         Lengo la Mpango huo ni kusimamia ukuzaji wa huduma za kifedha kwa jamii Nchini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Fedha. Vilevile, Mpango unalenga kusogeza huduma karibu kwa jamii pana zaidi ya Watanzania kwa kutumia mifumo ya Teknolojia mbalimbali katika kufikisha huduma  za  kifedha  kwa Wananchi na hasa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi waliopo Vijijini ambao wengi wao wako nje ya mfumo rasmi wa kifedha.  Teknolojia hizo ni pamoja na:
(a)          Huduma za Kibenki za moja kwa moja na kupitia Wakala (Agent Banking);
(b)          Huduma za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali kama vile M-PESA, TIGO PESA, AIRTEL MONEY na Easy PESA.
(c)          Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of Sales – POS).
19.         Aidha, Mpango huu utaweka mazingira linganifu na yaliyo bora kwa kutumiaSayansi na Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi, kuimarisha Sekta ya Fedha katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa ujumla. Mpango huu pia utawezesha kuongeza kasi ya upatikanaji wa Chakula, masuala ya Lishe na Maendeleo Vijijini kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
20.         Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika Nchi mbalimbali Barani Afrika unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo rasmi wa Taasisi za Kifedha ni Asilimia 24 tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi waliopo kwenye Mfumo rasmi wa Asasi za Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOs) ni Asilimia 22.  Asilimia 78 ya Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na wengi wao ni kutoka Vijijini hasa Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unalenga kufikia Asilimia 50 ya Watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha ifikapo mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika,
21.         Kiwango hiki kidogo cha Wananchi walio katika Mfumo rasmi wa huduma za kifedha unatokana na changamoto zifuatazo:
Moja:      Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha Vijijini ni hafifu hususan barabara, mawasiliano, makazi na huduma za kiusalama;
Mbili:       Wananchi wengi wa Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua umuhimu na faida ya huduma za kifedha.  Aidha, utamaduni wa kujiwekea akiba na kukopa ni mdogo; na.
Tatu:       Taasisi nyingi za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa Vijijini ambao ni Wakulima hawana fedha za kutosha kuweza kuweka akiba katika Taasisi hizo na uwezo wao wa kukopa mikopo ni mdogo, hivyo wakipeleka huduma zao huko hawatapata faida.
Mheshimiwa Spika,
22.         Zipo faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Wananchi wengi wa Vijijini hasa Wakulima.  Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:
Moja:         Kuwezesha Wananchi kujiwekea Akiba na pia kupata mikopo ya kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za kijamii hivyo kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;

Mbili:          Huduma za Kifedha Vijijini zinawawezesha Wananchi wengi hasa Wakulima kupata mikopo ya pembejeo na mikopo ya ununuzi wa mazao;

Tatu:          Huduma za Kifedha Vijijini ni Mkombozi wa Makundi maalum kama vile Vijana, Wanawake, Wazee, na Walemavu. Aidha, zinasaidia Wananchi kujiongezea kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki; na

Nne:           Kuwepo kwa Huduma za Kifedha Vijijini kunaongeza Usalama wa Chakula, kulinda mazingira na kufanya Vijiji kuwa ni sehemu nzuri ya kuishi.

Mheshimiwa Spika,
23.         Serikali imeonesha juhudi kubwa katika kuanzisha Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini kwa mfano tumeweza kuanzisha Benki nyingi Nchini.  Tayari tunazo Benki takriban 52 zenye matawi zaidi ya 609 kote Nchini.  Lakini pia tunazo huduma za Bima kwa Makampuni Binafsi zaidi ya 27 na Mawakala wa Bima takriban 600.  Ipo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Umma 5, Masoko ya Mitaji na Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban 5,600.

24.         Aidha tunazo huduma za Kifedha kwa kutumia Huduma za Kifedha kupitia mtandao (PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (POINTS OF SALES – POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo zaidi ya 55,000 ambapo Waajiriwa wa moja kwa Moja (Direct Employment) wanakadiriwa kufika takriban100,000.

Mheshimiwa Spika,
25.         Maisha bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na kutumia Teknolojia na kurahisisha maisha.  Kwa mfano, huduma za M-PESA peke yake zinawezesha malipo kwenye biashara mbalimbali zaidi ya aina 300 ikiwemo manunuzi kwenye Supermarket na maduka ya kawaida. Huduma hizo ambazo zinatolewa pia kwa njia ya TIGOPESA, AIRTEL MONEY, EASY PESA zinaweza kulipia Luku, Ada za shule na Vyuo, Tiketi za ndege, kufanya marejesho Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya Makampuni haya yameunganisha huduma zao na Benki zaidi ya20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard Chartered, Amana Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia huduma za jumuishi za kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka Akaunti ya Benki kwenda M- PESA, TIGO PESA n.k. halafu akazitoa kupitia Wakala.  Kwa sasa Watumishi walio Vijijini hawana tena sababu ya kufunga Ofisi kufuata mishahara Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha na wanaweza kutoa pesa kupitia Wakala, na kwa kufanya hivyo ufanisi na tija kwa Watumishi unaongezaka.

Mheshimiwa Spika,
26.         Ni kweli kwamba tunayo kazi kubwa ya kutekeleza Dhana ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini.  Lakini ni ukweli kuwa Uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha una  manufaa makubwa na mengi ikiwemo kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini  kwa kupeleka maendeleo Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo ya Milenia.  Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango huu utatuwezesha kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi.  Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za Kifedha na Vituo vya Kifedha kupitia mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala kuongeza jitihada katika kusambaza huduma za Kifedha Vijijini ambako ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi wanaohitaji huduma hiyo. 

IV:       NISHATI NA MADINI

a)            Mradi wa Gesi
Mheshimiwa Spika,
27.         Kama ambavyo Wananchi wengi wanafahamu, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafishia Gesi  Asilia  katika  maeneo  ya  Madimba, Mtwara Vijijini na Songo  Songo  Wilayani  Kilwa. Pia ujenzi wa Bomba la kusafirishia Gesi hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam unaendelea vizuri. Mradi huu utakapokamilika utaunganisha maeneo yanayozalisha Gesi Asilia hususan Mnazi Bay-Mtwara, Songo Songo, Kisiwani, Mkuranga, Ntorya na maeneo yaliyogunduliwa Gesi katika eneo la bahari ya kina kirefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi Asilia mbali na matumizi mengine, inatumika katika kuzalisha umeme ambao kwa sasa Asilimia kubwa unazalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta yanayoingizwa kutoka Nchi za nje na hivyo kuligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.



Mheshimiwa Spika,
28.         Katika utekelezaji wa mradi huu, Kazi zifuatazo zimekamilika hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2013:

Moja:        Kukamilika kwa upakuaji wa Shehena ya Sita (6) ya Mabomba ya Mradi yapatayo 4,444 ya umbali wa Kilomita 51.169 katika Bandari ya Mtwara. Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013 ni 24,935 ya umbali wa kilomita 295.5;

Pili:           Kusafisha Mkuza wa Mabomba, tayari Kilomita 498.5 zimekamilika;

Tatu:        Usafirishaji wa mabomba kutoka kwenye yadi za kuhifadhia na kuyasambaza kwenye Mkuza tayari kwa kuyaunganisha kwa kuchomelea. Hadi sasa mabomba ya Kilomita 186.9 yamekwishasafirishwa;

Nne:         Uchimbaji wa njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa Kilomita 27.0umekamilika;

Tano:       Uwekaji wa mabomba kwenye njia yake sambamba na kuweka Mkongo wa Mawasiliano (Fiber Optic Cable) umekamilika Kilomita 21.1;
Sita:          Kufukia bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano. Tayari   Kilomita7.30 za Bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano zimefukiwa; na

Saba:       Utafiti wa njia ya Bomba la Baharini nao umekamilika.
Hayo ni maeneo machache ambayo nimeona niyataje.

Mheshimiwa Spika,
29.         Ni kweli kwamba kazi za mradi huu ni kubwa lakini kwa ujumla zinaendelea vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo za mradi huu ambazo tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi wa Mradi ambao sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi wa Gesi na Mafuta.  Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi ni za kitaalamu sana, malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC) ni kuajiri wafanyakazi Wakiwemo Wazawa mapema ili waweze kushiriki na kujifunza kwa vitendo shughuli zote  zinazohusiana na ujenzi wa  mitambo na Bomba la Gesi hatua kwa hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa ujenzi. Utaratibu huu utasaidia kupata wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania watakaoendesha (operations) na kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi kwa kipindi chote cha matumizi.

Mheshimiwa Spika,
30.         Vilevile moja ya makubaliano katika Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huu, Mkandarasi anawajibika kuwapeleka Wafanyakazi kwenye mitambo na mabomba yanayofanya kazi  kwa sasa kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja  ili wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia shughuli zote za kuendesha mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi. Malengo ya TPDC ni kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti wakati wa kipindi cha ujenzi ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi Wafanyakazi wote wawe wamekwishapata uzoefu wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, 
31.         Kampuni nyingi zilizopo Mtwara zinazojishughulisha na mambo ya utafiti na uzalishaji wa Gesi na Viwanda vinavyohusiana na matumizi ya Gesi, zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa. Kwa mfano, Mpango wa kujenga mitambo ya kutengeneza  Gesi kuwa kimiminika (LNG) wa Kampuni ya British  Gas  Tanzania utakuwa  na  utengenezaji  wa ajira nyingi za kiwango kuanzia Kada ya Chini na Kada ya Kati ambayo  itasomesha Watanzania kupitia VETA katika fani mbalimbali. Wako watakaosomeshwa katika fani ya Vyuma, wengine ujenzi, uhandisi wa miundombinu na ufundi wa vyuma na umeme.

32.         Katika Kada ya Kati, Kampuni ya Gesi Tanzania wanatarajiwa kusomesha wataalamu 16,756 waliofaulu vizuri masomo ya Kidato cha Nne. Takwimu zinaonesha kuwa kwa Mtwara tu, kumekuwapo ajira mpya 400, na Watanzania wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta ni sawa na Asilimia 70 ya watoa huduma hiyo Nchini.  Asilimia 30 iliyobaki ya watoa huduma inatolewa na Wageni.

33.         Katika Kada za Juu, Kampuni itasomesha na kuajiri Wataalamu wa Jiolojia, Uhandisi, Kemia na Sayansi husika kwenye Gesi na Mafuta. Matokeo yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa VETA 370 wamesomeshwa kuhusu Gesi na Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa na Wanafunzi 12 wa Kada za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na Mafuta ndani na nje ya Nchi.

Mheshimiwa Spika,
34.         Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya British Gas Tanzania wamegundua gesi kiasi cha Futi za Ujazo Trilioni 13. Katika kuandaa na kuendesha mradi wa uzalishaji Gesi nyingi kiasi hicho ni dhahiri kwamba ajira zitapatikana kwa maelfu ya Watanzania. Katika hatua ya ujenzi, mradi utatoa ajira kwa maelfu; na katika uzalishaji (operations) ajira nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini, na katika mnyororo wa usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii kuwapa Watanzania matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa mengi sana, kuanzia upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha Wananchi wetu kuhusu manufaa ya mradi huu katika Nchi yetu.  Ni fursa ya kipekee ambayo Wananchi wetu wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha bora.

V:        MATUMIZI YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs)

Mheshimiwa Spika,
35.         Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Serikali ililiarifu Bunge lako Tukufu kuhusu mikakati mbalimbali itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devices- EFDs). Mashine hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata mapato stahiki bila udanganyifu. Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa kupitia Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye Hifadhi Kuu ya Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.

Mheshimiwa Spika,
36.         Katika utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka huu, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi 200,000 kati ya 1,500,000 ili waweze kutumia Mashine za Kielektroniki. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye biashara kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika zoezi hili, Wafanyabiashara Wadogo wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile Wamachinga na wale wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata kidogo.
Mheshimiwa Spika,
37.         Katika utekelezaji wa zoezi hili kumejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wafanyabiashara Nchini hususan wa Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na matumizi ya Mashine hizi. Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu: Bei kubwa ya ununuzi wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za kutolea Risiti; Mchakato uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa wa kutumia Mashine hizo; na Gharama za matengenezo.

Mheshimiwa Spika,
38.         Kwa kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba, Mashine za Kielektroniki zinafanya kazi zifuatazo:
Moja:              Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya kuandikia risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;

Pili:                 Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano;

Tatu:              Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi kisichopungua miaka mitano;

Nne:               Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;

Tano:             Mashine zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kumtaarifu Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;

Sita:                Kutuma na kupokea fedha kwa njia ya “Mobile Money”. Utaratibu huu unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia kodi na huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji, Simu, n.k;

Nane:             Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;

Tisa:               Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza Kodi halali.

Mheshimiwa Spika,
39.         Msingi wa bei ya kununulia Mashine hizi za Kielektroniki umezingatia pamoja na mambo mengine, manufaa na faida nyingi nilizozitaja kwa mtumiaji na ubora wa mashine zenyewe. Aidha, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali Duniani unaonesha kuwa mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo juu zinauzwa na wasambazaji kwa kati yaShilingi 600,000/= (Dola 375) hadi Shilingi 778,377/= (Dola 486) ikilinganishwa na bei za Mashine za Kielektroniki za Nchi nyingine zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania ambazo zinauzwa bei kubwa za kati ya Dola za Kimarekani 360hadi 870. Pamoja na bei hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana na Wasambazaji wa Mashine hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei hizo.

Mheshimiwa Spika,
40.         Kuhusu bei za karatasi za kutolea Risiti uchunguzi unaonesha kuwa karatasi hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/= hadi Shilingi 4,500/= kuzingatia ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo. Karatasi hizo zina uwezo wa kutoa wastani wa risiti kati ya Risiti 200 hadi 1,000 kulingana na urefu wa “Paper Roll”! au Bunda. Bei ya Karatasi hizi zinazojulikana kama “Thermal Paper” umezingatia kwamba ni za kisasa na hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza usalama.

Mheshimiwa Spika,
41.         Kuhusu utaratibu uliotumika kuwapata Watengenezaji na Wasambazaji wa Mashine hizi za Kielektoniki na Wasambazaji wa karatasi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa ushindani wa Kimataifa na haukuwa na dosari yoyote.

Mheshimiwa Spika,
42.         Katika kutafuta Watengenezaji na Wasambazaji, kwenye Awamu ya Kwanza Watengenezaji Wanne (4) na Wasambazaji Sita (6) walipatikana kwa kutumia Zabuni ya wazi ya Kimataifa (International Competitive Tendering) kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi Desemba Mwaka 2009 mpaka Mei 2010 makubaliano yaliingiwa kati ya kila Mtengenezaji na Msambazaji aliyechaguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya “Memorandum of Understanding (MOU).

43.         Kwenye Awamu ya Pili ya utekelezaji wa utaratibu huohuo wa Zabuni  ya Watengenezaji ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News, The African, Tovuti ya TRA na Tovuti ya PPRA.  Jumla ya Wazabuni Kumi na Nne (14) walituma maombi ambayo yalifunguliwa mara moja baada ya saa Nne asubuhi tarehe 27 Septemba 2012. Watengenezaji wa Mashine Wanne (4) walichaguliwa kati ya Kumi na Nne (14) waliokuwa wameomba na Wasambazaji Watano (5) walipatikana kati ya Tisa waliotuma maombi yao ndani ya muda. Kwa kifupi, huo ndio utaratibu uliotumika ambao ulikuwa wa wazi na ushindani. 

Mheshimiwa Spika,
44.         Ili kuhakikisha ubora wa Mashine hizi za Kielektroniki, Watengenezaji wametoa “Guarantee” ya muda wa miaka mitatu kwamba Mashine inayoharibika bila kukusudia na watawajibika kutoa mashine nyingine na pia kutoa elimu ya matumizi ya mashine hizo. Vilevile, kwa mujibu wa Mkataba ulioingiwa kati ya Wasambazaji na TRA, Wasambazaji wanawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo kila zinapoharibika ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji kutafuta watengenezaji wao wenyewe. Napenda kuwahakikishia Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na kuwawezesha kulipa kodi stahiki Serikalini.

Mheshimiwa Spika,
45.         Kwa kutambua umuhimu wa mashine hizi katika kuongeza Mapato ya Ndani; na ili kuyashughulikia malalamiko ya baadhi ya Wafanyabiashara yaliyojitokeza,Serikali imesogeza mbele muda wa mwisho wa kununua Mashine za Kielektroniki hadi tarehe 31 Desemba, 2013.  Lengo ni kuwawezesha Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa kununua mashine hizi na kujifunza namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi endelevu na faida za Mashine za Kielektroniki kwa Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na huduma. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Mfumo huu wa Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu na kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.

VI:       USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Mheshimiwa Spika,
46.         Tarehe 16 - 25 Oktoba 2013 nilifanya ziara ya kikazi Nchini China kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Keqiang. Katika ziara hiyo, nilifuatana na Viongozi wa Serikali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa Asasi za Sekta Binafsi Tanzania  na Watendaji Wakuu wa Serikali na Mashirika ya Umma ambao walishiriki kwenye mazungumzo na Wabia wetu kwa upande wa Jamhuri ya Watu wa China.

Mheshimiwa Spika,
47.         Dhamira kubwa ya ziara hiyo kimsingi ilihusu; kukuza mashirikiano ya kibiashara na utalii Nchini, kufanya mazungumzo na vyombo vya fedha ili kupata mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili marafiki, kuona Sekta Binafsi ya Tanzania inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa China na mwisho kutoa shukrani kwa misaada na mikopo ambayo Nchi yetu imepokea kutoka Jamhuri ya Watu wa China.

Mheshimiwa Spika,
48.         Kama mnavyojua Taifa la Jamhuri ya Watu wa China ni miongoni mwa Nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na limepiga hatua kubwa sana katika maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika Taifa la China, nilitoa mwaliko wa kuwakaribisha ili kushirikiana na Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wake katika Nyanja za kiuchumi, utamaduni na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na soko kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.
Mheshimiwa Spika,
49.         Katika ziara hiyo nilipata fursa ya kutembelea Miji ya Beijing, Shenzhen, Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata nafasi ya kukutana na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China. Kutokana na Mikutano hiyo, baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma wameanza kuja Nchini kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ili kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi.  

Mheshimiwa Spika,
50.         Kwa ujumla ziara hii ilikuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano, pamoja na kuendeleza na kudumisha ushirikiano ambao umeanzishwa na Viongozi waasisi wa Nchi hizi mbili yaani Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong wa Jamhuri ya Watu wa China, kwenye ziara hiyo, niliweza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Bwana Li Keqiang, pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China. Ninaamini tukijipanga vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.



Mheshimiwa Spika,
51.         Ziara yangu pia ilifanikisha kutiwa saini kwa Mikataba ya ushirikiano wa Tanzania na China katika eneo la Sayansi na Teknolojia na katika Utalii.  Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu uuzaji wa bidhaa za baharini za Tanzania Nchini China na kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao la Pamba Nchini. Aidha, Mikataba ya Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na Makazi baina ya Makampuni ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya Umeme - TANESCO, Shirika la Taifa la Maendeleo - NDC na Shirika la Taifa la Nyumba - NHC ilisainiwa.

Mheshimiwa Spika,
52.         Mafanikio mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuyashawishi Makampuni makubwa ya usafiri wa anga na Mawakala wa safari za kitalii kuwekeza Tanzania.Katika jitihada hizo nilikutana na Makampuni ya China Hainan, China Southern Air Line Holding Company na China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited.
53.         Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa kiasi kikubwa Makampuni haya ya Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha utayari wao wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na China.  Aidha, Kampuni yaChina Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited ambayo inafanya biashara ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali duniani wameonesha nia ya kuja kuwekeza hapa Nchini katika Sekta ya Hoteli kubwa za Kitalii. Kampuni ya China Merchants Holdings International Limited ambayo imehusika katika ujenzi wa Bandari kubwa na Mji wa Shenzhen katika Jimbo la Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia ubia na Serikali yetu katika ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na Mji wa Bagamoyo unaotarajiwa kuwa “Trade Hub” ya Afrika.